Kwa mujibu wa shirika la habari la ABNA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria katika taarifa yake ililaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni katika majimbo ya Quneitra na Daraa, na kuyataja kuwa ukiukaji wa wazi wa mamlaka na uadilifu wa ardhi ya nchi hiyo.
Katika taarifa hiyo imeelezwa kwamba mashambulizi ya mizinga na uvamizi wa wanajeshi wa Israel katika ardhi ya Syria, pamoja na kueneza hofu na woga miongoni mwa raia, yanakinzana na sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Makubaliano ya Kutenganisha Vikosi ya mwaka 1974.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilisisitiza: Kuendelea kwa uchokozi huu kunatishia usalama na utulivu wa eneo hilo na kuongeza mateso kwa wakazi wa maeneo ya mpakani.
Damascus pia iliomba Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yao na kuchukua hatua za kukomesha uchokozi unaorudiwa wa utawala wa Kizayuni na kuhakikisha utekelezaji kamili wa Makubaliano ya Kutenganisha Vikosi.
Kwa mujibu wa ripoti, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni Jumapili waliingia katika kijiji cha Abidin kilicho magharibi mwa mji wa Daraa na kulishambulia eneo hilo kwa helikopta na mizinga, na kusababisha uharibifu wa nyumba za makazi na kulazimisha wakazi kadhaa kuondoka katika nyumba zao.
Your Comment